1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa mamlaka ya Wapalestina aidhinisha serikali mpya

Bruce Amani
28 Machi 2024

Mamlaka ya Palestina imetangaza baraza jipya la mawaziri huku ikikabiliwa na shinikizo la kimataifa la kufanya mabadiliko. Rais Mahmoud Abbas wa mamlaka hiyo ameitangaza serikali hiyo mpya kutokana na amri ya rais.

https://p.dw.com/p/4eEIi
Mohammad Mustafa (Kushoto) na Mohammed Mustafa (Kulia)
Serikali mpya ya Mamlaka ya Wapalestina imeidhinishwa ikiwa na jukumu la kumaliza vita vya GazaPicha: Palestinian President Office/Xinhua/picture alliance

Katika makao makuu ya Ukingo wa Magharibi, mjini Ramallah, Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas leo ameridhia serikali mpya iliyoundwa na Waziri mkuu Mohammed Mustafa, ambayo wanachama wake wanatarajiwa kuapishwa Jumapili. Mustafa amesema kipaumbele cha kitaifa kwa serikali hiyo mpya ni kumaliza vita vya Gaza, akiongeza kuwa baraza lake la mawaziri litafanya kazi ya kuyaweka maono ya kuziunganisha taasisi, ikiwemo kuchukua majukumu kwa ajili suala la Gaza.

Soma pia: Rais Abbas amteua mchumi kuwa Waziri Mkuu wa Palestina

Mawaziri wote aliowataja hawana umaarufu mkubwa. Karibu watano kati ya mawaziri 23 wanaoingia serikalini wanatokea Gaza ingawa haijajulikana iwapo bado wapo katika eneo hilo. Tafiti za maoni za miaka ya hivi karibuni zimeonesha kwamba Wapalestina walio wengi wanamtaka Abbas mwenye umri wa miaka 88 aachie ngazi. Mamlaka ya Palestina inasimamia sehemu ya Ukingo wa magharibi unaokaliwa na Waisraeli. Haina mamlaka Gaza baada ya majeshi yake kufukuzwa  pale kundi la hamas lilipochukua madaraka mwaka 2007. Wapalestina wachache ndio wanaoiunga mkono mamlaka hiyo sababu moja ikiwa kutofanya uchaguzi katika kipindi cha miaka 18

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

Kwingineko, Ufaransa imetangaza kuwa itatoa mwaka huu euro milioni 30 kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi wa Kipalestina – UNRWA ili kusaidia operesheni zake katika wakati huu wa vita vya Gaza.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Christophe Lemoine amewaambia waandishi Habari mjini Paris kuwa watatoa mchango wao wakati wakihakikisha kuwa masharti yanatimizwa kwa UNRWA kutekeleza majukumu yake katika hali isiyokuwa na uchochezi wa chuki na machafuko.

Familia za wanajeshi waliotekwa kukutana na Netanyahu

Israel | Vita kati ya Israel na Hamas
Familia za raia wa Israel waliotekwa na wanamgambo na kupelekwa Gaza zinashinikiza waachiliwe huruPicha: Nir Alon/ZUMA Press Wire/picture alliance

Wakati hayo yakijiri, familia za wanajeshi wanaoshikiliwa mateka huko Gaza zimesema zinatarajiwa kukutana leo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa mara ya kwanza tangu Oktoba 7 wakati wapendwa wao walipotekwa nyara na kupelekwa Gaza. Daniel Neutra, ni kaka ya Omer, raia wa Marekani mwenye asili ya Israel, anayeshikiliwa mateka Gaza.

"Katika mkutano wetu, tunataka kujua kuna mpango gani wa kuwarudisha nyumbani, na tunataka waachiliwe mara moja, sasa hivi, kutoka kwa Waziri Mkuu. Umekuwa muda mrefu, na namhitaji kaka yangu."

Mjini Rafah, ambako zaidi ya watu milioni moja wamepewa hifadhi, maafisa wa afya wamesema shambulizi la angani la Israel kwenye nyumba moja limewauwa watu wanane na kuwajeruhi wengine.

Jeshi la Israel lakabiliana vikali na wanamgambo 

Wakazi karibu na hospitali ya Gaza walishauriwa kuondoka
Makabiliano makali yamekuwa yakiendelea katika hospitali ya Al-Shifa kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgamboPicha: Dawoud Abo Alkas/Anadolu Agency/picture alliance

Wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Kipalestina wamekabiliana vikali karibu na hospitali ya Al Shifa huko Gaza, ambako wapiganaji wa Hamas na Islamic Jihad wamesema waliwashambulia askari wa Israel na vifaru kwa kutumia maroketi na mizinga. 

Jeshi la Israel limesema linaendelea na operesheni yake karibu na eneo la hospitali ya Al-Shifa katika mji wa Gaza baada ya kuivamia zaidi ya wiki moja iliyopita. Wanajeshi wake wamesema wamewauwa karibu wanamgambo 200 tangu kuanza kwa operesheni hiyo, wakati wakizuia madhara kwa raia, wagonjwa, timu za madaktari, na vifaa vya matibabu.

Matawi ya kijeshi ya Hamas na Islamic Jihad yamesema katika taarifa kuwa yaliiripua, kwa kutumia mfululizo wa makombora, mikusanyiko ya wanajeshi wa Israel katika eneo la hospitali ya Al-Shifa katika operesheni ya pamoja.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani – WHO Tedros Adhanom Gebreyesus ameandika kwenye mtandao wa X kuwa kwa mara nyingine WHO inataka kusitishwa mara moja kwa mashambulizi ya hospitali huko Gaza, na unatoa wito wa ulinzi wa wahudumu wa afya, wagonjwa, na raia.

Reuters, afp